Saturday, April 28, 2012
Umuhimu wa kula Matunda
Matunda yana faida nyingi mwilini na ni miongoni mwa vyakula vinavyopaswa kupewa kipaumbele katika milo yetu ya kila siku. Lakini kwa bahati mbaya, siyo watu wote wanaelewa umuhimu wa matunda na jinsi ya kula ili kupata faida zake.
Kutokana na kula matunda kinyume na utaratibu, watu wengi huyachukia matunda baada ya kujikuta wakiumwa tumbo au kujisikia kichefuchefu na kutapika mara baada ya kula. Wengine husikia tumbo kujaa gesi na kusikia kiungulia.
Halikadhalika, watu wengi wamefundishwa na kuzoeshwa kulishwa matunda baada ya mlo, mazoea ambayo ni kinyume kabisa na kanuni za ulaji sahihi wa matunda. Katika makala haya, utaelewa njia sahihi ya kula matunda ili kupata faida zake.
KULA MATUNDA TUMBO LIKIWA TUPU
Ili kunufaika na matunda, kula matunda wakati ukiwa na njaa na tumbo likiwa tupu. Unapokula matunda katika hali hii, matunda husagika haraka na virutubisho vyake husambaa mwilini kwa urahisi. Baada ya saa moja au zaidi, unaruhusiwa kula mlo wako mwingine kama kawaida.
USILE BAADA YA KULA
Imezoeleka na watu wengi kula matunda baada ya mlo kamili. Hata kwenye hafla na tafrija kubwa mbalimbali, utaona matunda huliwa mwishoni baada ya chakula. HII SIYO SAHIHI na hayo ni makosa miongoni mwa makosa mengi yanayofanyika kwa sababu ya mazoea tu.
Inaelezwa kuwa ulaji wa matunda baada ya mlo siyo sahihi kwa sababu matunda huyeyuka haraka kuliko chakula cha kawaida. Tunda linapokuwa tayari kupita tumboni kuelekea kwenye utumbo mwembamba, huzuiwa na chakula. Baada ya muda tunda linachanganyika na chakula na kuoza na hatimaye kuzalisha asidi ambayo humfanya mtu kuumwa tumbo baada ya kula matunda. Lakini pia virutubisho vyake hupotea.
Ili kuepukana na hali hiyo ya msongamano kwenye tumbo, kula matunda saa moja kabla au kama utakula baada ya mlo, angalau kula baada ya masaa mawili. Ukila baada ya muda huo, utakuwa umetoa nafasi ya chakula kusagika na bila kuzuia uyayukaji wa matunda.
ZINGATIA KIWANGO CHA SUKARI KWENYE MATUNDA
Baadhi ya matunda, kama vile papai, ndizi mbivu, yana kiwango kingi cha sukari, karibu matunda yote yana sukari, lakini mengine huwa na kiwango kingi zaidi. Hivyo inashauriwa kula matunda kwa kiwango cha wastani kila siku bila kuzidisha kiwango cha sukari cha gramu 25 kinachohitajika kwa siku.
Aidha, unapokula tunda, hakikisha unakula tunda kwa ukamilifu wake ili kupata virutubisho vyote. Kwa mfano unapokula chungwa, ni vizuri pia ukala pampoja na nyama zake ili kupata virutubisho vyote muhimu vilivyomo.
Jiwekee tabia ya kula matunda ya aina mbalimbali kwa nyakati tofauti ili kupata vitamini na madini tofauti tofauti kulingana na mahitaji ya mwili. Kwa kuwa matunda ndiyo yanayojenga na kuimarisha kinga ya mwili, ulaji wa matunda ya aina mbalimbali kutakuhakikishia mwili wako kinga imara dhidi ya maradhi na kamwe hutasumbuliwa na magonjwa mara kwa mara.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.